Jumapili 14 Juni 2026 - 09:00
Serikali ya Lebanon Imesimama Pamoja na Muqawama au Pamoja na Israel?

Hawza/ Ahmad Varol, mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Uturuki, amekosoa misimamo ya serikali ya Lebanon kuhusu Hizbullah na Iran, akisisitiza kwamba viongozi wa Lebanon, badala ya kukabiliana na mashambulizi ya Israel, wamechukua mkondo wa kuongeza shinikizo dhidi ya mkondo wa Muqawama.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Islamic Analysis, mwandishi na mchambuzi wa Uturuki Ahmad Varol, katika makala yake, aliikosoa misimamo ya hivi karibuni ya maafisa wa Lebanon kuhusu Hizbullah na Iran. Aliitupia lawama serikali ya Lebanon kwa kuchukua mtazamo wa kujihami na kutofanya chochote mbele ya Israel, na akauliza: “Je, ni kweli mnaitetea Lebanon au mnawatetea wavamizi wa Kizayuni?”

Varol, katika makala yenye kichwa cha habari kisemacho “Je, ninyi ni wamiliki wa nchi au walinzi wake?”, aliandika kwamba; watawala wa nchi si wamiliki wa ardhi zao, bali ni watu wenye jukumu la kulinda haki za wananchi na uadilifu wa mipaka ya nchi zao.

Katika muktadha huo, alirejelea kauli za hivi karibuni za Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, ambaye alikuwa amesema akiwaelekea Hizbullah na Iran:

“Hii si nchi yenu; hii ni nchi yetu.”

Kwa mtazamo wa mwandishi huyo, Lebanon si mali ya Joseph Aoun, si ya Hizbullah wala si ya Iran, bali ni mali ya watu wake. Na viongozi wa Lebanon wana wajibu wa kutetea haki za wananchi dhidi ya mashambulizi ya Israel.

Varol alikosoa pia utendaji wa serikali ya Lebanon katika mazungumzo ya usitishaji vita yaliyofanyika kwa upatanishi wa Marekani. Alidai kwamba ujumbe wa Lebanon katika mazungumzo hayo haukuchukua msimamo thabiti na wenye heshima, na kwamba jeshi la Lebanon pia halikuonyesha radi amal yenye ufanisi dhidi ya mashambulizi na kusonga mbele kwa vikosi vya Israel.

Aidha, alirejelea kauli ya Waziri Mkuu wa Lebanon aliyoiambia Iran, ambapo alitaka kusitishwa kwa matumizi ya kusini mwa Lebanon kama “nyenzo ya kujadiliana na kufanya biashara ya kisiasa”.

Varol alijibu kwa kuandika kwamba; ikiwa kuna haja ya kuomba huruma kwa ajili ya watu wa kusini mwa Lebanon, basi ombi hilo linapaswa kuelekezwa kwa Israel kama upande unaofanya mashambulizi, si kwa Iran.

Mchambuzi huyo wa Kituruki, akizungumzia makubaliano ya usitishaji vita kati ya Lebanon na Israel, alisema kwamba; Israel haijazingatia hata moja ya makubaliano hayo, aliongeza kuwa; hata baada ya makubaliano ya mwisho, Israel iliendelea na mashambulizi yake ya anga.

Kwa mujibu wake, Iran pia, katika kujibu mashambulizi hayo na kwa lengo la kuilazimisha Israel kusitisha uchokozi wake dhidi ya Lebanon, ililenga maeneo ya ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwa kutumia makombora ya balestiki.

Mwishoni mwa makala yake, Varol aliwauliza viongozi wa Lebanon swali hili: “Katika hali ambayo wananchi wa Lebanon wanakabiliwa na tishio linalotokana na sera za upanuzi na uchokozi wa Kizayuni, je, ninyi mnaitetea Lebanon au kwa vitendo mmesimama upande wa wavamizi wa Kizayuni?”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha